Serikali imeondolea mbali gharama za matibabu kwa wote waliojeruhiwa kwenye maandamano yalioshuhudiwa hivi majuzi,hatua ambayo inalenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia zao.
Kwenye taarifa Jumatatu,waziri wa afya Aden Duale aliagiza Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), kugharamia malipo ya matibabu kwa wote waliofikishwa kwenye hospitali hiyo kwa matibabu kufuatia maandamano hayo kwa kutumia hazina yake ya mikasa.
Wizara ya afya pia iliahidi kuwasaidia wote ambao bado wanauguza majeraha waliopata kufuatia maandamano hayo.
“Nimeagiza usimamizi wa Hospitali Kuu ya kenyatta kufutilia mbali bili za matibabu kwa wagonjwa waliojeruhiwa wakati wa maandamano, bili hizo zilipwe kupitia hazina ya mikasa ya dharura,” aliagiza Duale.
Agizo hilo linajumuisha malipo ya matibabu kwa marehemu Boniface Kariuki ambayo yalitimia takriban shilingi 815,805 alipofariki siku ya jumatatu alasiri.