Seneti yaanza kujadili kubanduliwa kwa Gavana Guyo

Gavana huyo wa Isiolo alibanduliwa madarakani Alhamisi kwa madai ya kukiuka maadili na matumizi mabaya ya mamlaka.

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la Seneti linaandaa kikao maalumu leo Jumatatu Juni 30, 2025 kujadili hoja ya kubanduliwa mamlakani kwa Gavana wa kaunti ya Isiolo Abdi Ibrahim Hassan Guyo.

Wanachama wa bunge la Kaunti ya Isiolo walipiga kura ya kumbandua Guyo Alhamisi Juni 26, 2025 ambapo 16 kati ya wote 18 waliunga mkono hoja hiyo.

Ijumaa bunge la Seneti lilifahamishwa rasmi kuhusu hatua hiyo ndiposa Spika Amason Kingi akatenga leo Jumatatu kuwa siku ya kusikiliza hoja hiyo kuanzia saa nne asubuhi.

Guyo analaumiwa kwa ukiukaji wa maadili na matumizi mabaya ya mamlaka ambapo mwasilishi wa mjadala wa kumbandua ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Sericho Abubakar Godana, alisema Gavana ameshindwa kuafikia malengo ya ukusanyaji ushuru.

Godana anadai pia kwamba Gavana Guyo amezidisha mara dufu idadi ya wanachama wa kamati kuu ya kaunti (sawa na mawaziri) ambao ni 36 na maafisa wakuu ni 31.

Kiongozi huyo analaumiwa pia kwa kuwapa watumishi wakuu wa kaunti kandarasi ya miaka miwili pekee hatua inayodhoofisha usalama wa ajira zao na uwajibikaji. Alitoa kandarasi mpya kwa watumishi watano pekee kati ya 20 ambao kandarasi zao zilifikia kikomo.

Hatima ya Gavana Guyo ambaye amekanusha madai yote dhidi yake sasa iko mikononi mwa bunge la Seneti ambalo litaamua katika kikao cha leo iwapo litasikiliza madai dhidi yake kama bunge zima au kuteua kamati ya wanachama 11 kufanya hivyo.

Share This Article