Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula Jumapili alitawazwa rasmi kama mzee wa heshima na jamii ya Samburu katika mji wa Maralal.
Hafla hiyo, iliyoandaliwa na baraza la wazee wa Samburu, ilifanyika katika eneo la Horr Kusini, Kaunti ya Samburu, ambapo taratibu za kitamaduni, nyimbo, maombi na baraka zilifanyika kumtambua Spika Wetang’ula kwa kujitolea kwake kuendelea kutetea jamii zilizotengwa hasa wafugaji, utawala bora, ustawishaji wa amani na maendeleo ya kimaeneo.
Baraza hilo lilimkabidhi Spika Wetang’ula rungu la shanga na pembe ya ng’ombe ishara za uongozi, mwongozo na hadhi ya uzee katika utamaduni wa jamii ya Samburu.
Chifu Simon Lemboyok mwanachama wa baraza la wazee wa Samburu alisema kutambuliwa kwa Wetang’ula kama mzee wa heshima ni kielelezo cha juhudi zake thabiti za kuendeleza amani, kuunga mkono elimu na kuimarisha ushirikiano kati ya kaunti—maadili yanayokubalika sana na jamii ya Samburu.
Katika hotuba yake ya kukubali heshima hiyo, Spika Wetang’ula alizungumzia uhusiano wa karibu kati ya jamii za maeneo mbalimbali na taasisi za kitaifa za Kenya kwa kusema:
“Kupokelewa kama mzee wa heshima na watu wa Samburu ni jambo la unyenyekevu na la kutia moyo. Ninaahidi kuheshimu mila zenu, kuendeleza maadili ya uongozi wenu wa jadi na kusalia kuwa mtetezi wa amani na maendeleo jumuishi” alisema.
Wetang’ula alisisitiza kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono vipaumbele vya kimaeneo kama uhifadhi wa urithi wa kitamaduni, uboreshaji wa usalama katika maeneo ya wafugaji na upatikanaji wa elimu.
Aliahidi kuwa mtetezi thabiti wa jamii za wafugaji na kuunga mkono miradi inayolenga kuboresha maisha katika maeneo kame na ya ukame wa wastani.
Spika alikuwa ameandamana na Gavana wa Samburu Jonathan Lati Lelelit, Gavana wa zamani wa Samburu Samuel Lenolkulal, Mbunge wa Samburu Kaskazini Dominic Eli Letipila, Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Laikipia Jane Kagiri, Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda na Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera kati ya wengine wengi.