Msanii wa muziki nchini Tanzania Diamond Platnumz amemhakikishia mfuasi wake sugu Baba Levo uungwaji mkono katika safari yake ya kuwania ubunge wa eneo la Kigoma Mjini.
Diamond ambaye yuko kwenye ziara nchini Ufaransa alichapisha picha ya Baba Levo akikabidhiwa fomu za kuomba kuwania ubunge kupitia chama cha CCM na kuandika, “Najua ni kiasi gani unaipenda na una uchungu na Kigoma”.
Ikumbukwe kwamba Baba Levo aliwahi kujaribu muziki na alikuwa mmoja wa sanii walioimba wimbo wa Kigoma All Stars ambapo Diamond Platnumz naye alikuwa na hivyo urafiki wao ni wa muda mrefu.
Katika ujumbe wake Diamond alitaja jinsi Baba levo amekuwa akipambania eneo la Kigoma kwa hali na mali na kwamba siku moja alimwambia kwamba siku akijaliwa kuwa mbunge, atahakikisha Kigoma inapata maendeleo stahiki.
“Ninakuamini na nikuthibitishie tu kwamba kwenye hili la ubunge una uungaji mkono wangu kwa hali na mali kuhakikisha Kigoma yetu inapata maendeleo” alimalizia Diamond.
Mwingine ambaye Diamond amemhakikishia uungwaji mkono wa hali na mali ni Romy Jons au RJ The Dj ambaye ni kakake aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania ubunge wa eneo la Mbagala.
Msanii huyo ameahidi pia kumuunga mkono Romy Jons ili kuhakikisha anahudumia watu wa Mbagala ipasavyo na kuwaletea maendeleo.
“Labda tu chama kisikupe nafasi” alisema Diamond katika ujumbe wake kwenye Insta Stories ishara ya imani kubwa aliyo nayo ya kakake kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.