Bunge lijalo la Tanzania huenda likawa na wasanii na washawishi wa mitandaoni wengi, ikitizamiwa idadi yao ambao wanaendelea kuchukua fomu za kutafuta kuchaguliwa.
Tanzania inatizamiwa kuandaa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025 na watu wengi wameonekana wakichukua fomu za kuwania nyadhifa mbali mbali.
Wa hivi punde zaidi kuchukua fomu ya chama cha CCM ni mfanyabiashara na mwanamuziki Zuena Mohamed maarufu kama Shilole au Shishi Baby ambaye alichukua fomu ya kutafuta kuteuliwa kwa viti maalum katika mkoa wa Tabora.
Msanii huyo alichapisha picha inayomwonyesha akiwa na fomu hiyo na kuandika, “Namshukuru Mwenyezi Mungu mapema leo nimefanikiwa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama changu cha CCM kugombea nafasi ya UBUNGE wa Viti maalumu mkoa wa Tabora”.
Mtangazaji na mshawishi wa mitandaoni Mwijaku ambaye jina lake halisi ni Burton Mwemba naye alichukua rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge wa eneo la Mvomero katika mkoa wa Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi – CCM.
Mtani wake pia ajulikanaye kama Baba Levo au kwa jina rasmi Clayton Revocatus Chipando naye alitagaza kupitia Instagram kwamba ameshachukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa eneo la Kigoma Mjini.
Mchakato mzima wa kuchukua fomu, kuijaza na kuirejesha ulimchukua mkereketwa huyo wa Diamond Platnumz dakika 17 pekee.