Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ameshukuru raia wa nchi hiyo hasa wanachama wa chama chake cha National Resistance Movement NRM kwa kuunga mkono azma yake ya kuwania Urais kwa mara nyingine.
Museveni ambaye anatafuta muhula wa saba uongozini katika uchaguzi mkuu unaopangiwa kuandaliwa Januari 2026, jana alichukua fomu za kuwania uenyekiti wa chama cha NRM na Urais.
Kiongozi huyo huenda akaendeleza muda wake katika uongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki hadi miaka 45 iwapo atafanikiwa kuchaguliwa tena na hivyo kuwa kati ya marais watano waliohudumu kwa muda mrefu zaidi ulimwenguni.
Akihutubia umati katika hafla ya shukrani ya spika wa bunge la Uganda Anita Among, Museveni alishukuru wananchi kwa kuunga mkono azma yake ya kuwania tena urais.
“Ningependa kushukuru watu wa Teso na watu wote wa Uganda kwa kuunga mkono NRM na kupendekeza kwamba niwe mwenyekiti wa NRM kwa miaka mitano zaidi na mwaniaji wa Urais wa chama hicho,” alisema Rais Museveni.
Rais Museveni aliingia kwenye uongozi wa Uganda Januari 29, 1986, baada ya kuongoza mchakato uliofanikiwa wa miaka mitano wa kupambania ukombozi wa Uganda.
Amekuwa Rais kwa miaka 39 sasa, hali iliyowezeshwa na mabadiliko mawili yaliyofanyiwa katiba ya Uganda, la kwanza la mwaka 2005 ambalo liliondoa kikwazo cha idadi ya mihula ambayo mtu anaweza kuhudumu kama Rais.
Badiliko la pili lilifanywa mwaka 2017 na kuondoa kikwazo cha umri wa mtu anayetaka kuwania Urais na anayeruhusiwa kuendelea kuwa Rais.