Washukiwa 24 wakamatwa kuhusiana na ghasia wakati wa maandamano

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa 24 wakamatwa Kikuyu kwa madai ya kusababisha ghasia wakati wa maandamano.

Maafisa wa polisi kaunti ya Kiambu, wamewakamata washukiwa 24 kuhusiana na ghasia zilizozuka wakati wa maandamano ya Gen Z mnamo Juni 25,2025.

Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, washukiwa hao ambao wanadaiwa kupatikana na mali ya wizi, walifikishwa kwenye mahakama ya Ruiru, ambayo iliagiza wazuiliwe kwa siku 14 kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi.

“Maafisa wa upelelezi wanaendelea na uchunguzi kuwatia nguvuni washukiwa zaidi waliohusika na kwenye ghasia hizo,” ilisema DCI kupitia ukurasa wa X.

Aidha baadhi ya mali iliyoibwa kutoka afisi za serikali ya kaunti ya Kiambu zilipatikana katika maeneo ya Mai-ii-hii na kabete. Mali hiyo ni pamoja na rukwama, milango na enki ya kuhifadhi maji.

Huduma ya Taifa ya Polisi imetoa wito kwa umma kujiepusha na uharibifu wa mali wakati wa maandamano, ikisema hatua hiyo itakabiliwa vilivyo.

TAGGED:
Share This Article