Naibu Rais Kithure Kindiki amesama uvamizi kwenye vituo vya polisi, wizi wa bunduki na risasi na uteketezaji wa majengo ya serikali ni sawa na ugaidi na waliopanga, kufadhili na kutekeleza maovu hayo watachukuliwa hatua kali.
Alisema hatua ya kuyumbisha taifa hili jinsi ilivyoshuhudiwa Jumatano, hazitavumiliwa na waliohusika watachukuliwa hatua.
“Ikiwa ulihusika katika visa hivi vya ugaidi na uhalifu, tutakukamata. hatutasubiri usababishe maafa zaidi na uharibifu,” alisema Kindiki.
Akizungumza Ijumaa wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake, vijana na wafanyabiashara wadogo katika kaunti ya Kitui, Prof. Kindiki alidokeza kuwa maandamano hayo yalitekwa na wahalifu waliokuwa na nia potovu.
Kindiki alisema kuwa maandamano ya vijana waliokuwa wakitoa wito wa utumizi bora wa rasilimali za serikali, ulitekwa na wahalifu waliosababisha ghasia na mashambulizi dhidi ya vifaa vya serikali.
“Visa hivyo havitatokea tena,” alithibitisha Kindiki.
Huku akihakikisha utiifu wa katiba na uhuru uliobainishwa, Naibu huyo wa Rais alionya dhidi ya udhalalishaji wa usalama wa taifa.