Rais William Ruto ametoa wito kwa wananchi kuheshimu na kushirikiana na huduma ya taifa ya polisi kabla ya maandamano ya vijana ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z kushuhudiwa nchini.
Rais Ruto aliwaonya wahalifu dhidi ya kuwatishia au kuwashambulia maafisa wa polisi.
Akiongea katika Ikulu ya Nairobi wakati wa dhifa ya kiamsha kinywa iliyoandaliwa kwa heshima ya timu za Kenya Police FC na Kenya Police Bullets kwa kushinda taji za Ligi Kuu ya FKF mwaka huu, kiongozi wa taifa alisema serikali yake itaendelea kuwaunga mkono maafisa wa usalama waliojitolea kulinda maisha na mali ya Wa-Kenya.
“Tutawaunga mkono maafisa wa polisi, wao ni nguzo muhimu kwa udhabiti na ustawi wa taifa hili,” alisema Rais Ruto.
Alisema bila amani na usalama, nchi hii haitaendelea. Rais Ruto alisema vitengo vya usalama vinahitaji usaidizi wa kutosha ili kulinda taifa hili.