Mwimbaji wa Uganda Daudi Mugema anaripotiwa kuaga dunia katika mazingira tatanishi katika chumba cha hoteli alichokuwa amekodisha mjini Gulu, kaskazini mwa Uganda.
Mugema ambaye wengi wanamfahamu kwa wimbo wake uitwao “Katonda W’abanaku” alikuwa amesafiri hadi Gulu kwa lengo la kukutana na General Salim Swaleh.
Inaaminika msanii huyo ambaye amekuwa akiugua saratani kwa muda alikuwa amekwenda kutafuta usaidizi wa kifedha kutoka kwa Swaleh ambaye ni kakake Rais Museveni ili aendeleze matibabu yake.
Mwanzo wa mwaka huu, Mugema alilazwa hospitalini akiwa amevimba miguu na kulingana naye, madaktari wa hospitali ya Mulago walithibitisha kwamba anaugua saratani.
Hata hivyo, uchunguzi wa ziada aliofanyiwa katika hospitali tatu jijini Istanbul nchini Uturuki ulikuwa na matokeo kinzani kwamba hakuwa na saratani.
Safari ya Mugema hadi Uturuki ilifadhiliwa na watu kadhaa wenye nia njema wakiwemo General Salim Swaleh, Meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago, Stabua Natooro, Haruna Kyeyune Kasolo, Lule, Hajji Haruna Mubiru, Mesach Semakula, Eddy Kenzo, David Lutalo na Mama Fiina.