Rachel Ruto: Serikali imejitolea kuwawezesha wajane

Tom Mathinji
2 Min Read
Mama Taifa Rachel Ruto.

Mama Taifa Rachel Ruto siku ya Jumatatu aliwaongoza Wakenya katika maadhimisho ya 21 ya siku ya kimataifa ya wajane, huku akitoa ujumbe wa kuhakikisha maisha yenye heshima na ujumuishaji wa kiuchumi.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Buga, kaunti ya Nyamira, Mama Taifa alihakikisha kujitolea kikamilifu kwa serikali kuwawezesha wajane kote nchini, akisisitiza kumujuishwa kwao na wala sio kuwatenga.

“Nina furaha kwamba serikali imepiga hatua. Kupitia Hazina ya Hustler na mipango ya wanawake ya kiuchumi, zaidi ya wajane 15,000 wamepata fedha za kuanzisha biashara. Zaidi ya wanawake 2,000 wamepata zabuni za serikali kupitia vyeti vya AGPO na kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa taifa,” alisema Rachel Ruto.

“Kuwawezesha kiuchumi pekee hakutoshi. Lazima tukabiliane na tamaduni zinazowakosesha heshima wajane,” alihimiza Mama Taifa huku akitoa wito kwa jamii kuwakumbatia wajane na kuwaunga mkono badala ya kuwatenga.

Aidha aliwahimiza wajane kujiunga na vikundi ili kunufaika na hazina zilizopo za kiuchumi ambazo zimeanzishwa na serikali kuanzia viwango vya wadi hadi kitaifa.

“Ni vizuri kina mama tuweze kuingia katika vikundi, ili vikundi hivi viweze kuwahudumia. Serikali ina mipango mingi ambayo inaweza kusaidia akina mama. Tuingie vikundi na tusivunje vikundi,” alisema Mama Taifa.

“Serikali yetu, inayoongozwa na Rais William Ruto, inawajali wajane. Jambo muhimu kwa akina mama ni kwamba, ikiwa utasikia kuna jambo ambalo serikali inafanya, tafadhali jihusishe na hilo jambo,” aliongeza Rachel Ruto.

kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya wajane mwaka huu ni, ‘Mwezeshe: Kutoka Kupoteza Hadi Uongozi’.

Share This Article