Joycelyn Savage, mchumba wa mwanamuziki anayezuiliwa R. Kelly, amejitokeza kukanusha madai ya familia yake kwamba yeye ni mmoja wa wahanga wa mwanamuziki huyo.
Savage alichapisha video Jumapili jioni, ambapo anaonekana akikanusha kabisa madai kwamba yeye ni mtumwa wa kingono wa mwanamuziki huyo.
Alichukua hatua hiyo siku chache baada ya wazazi wake kuhojiwa na kupinga wazo lolote la kuachiliwa kwa Kelly wakisema bado anadhibiti binti yao ambaye ni mmoja wa watumwa wake wa kingono.
Joycelyn alisema kwamba yeye na R. Kelly wamekuwa pamoja kwa miaka 10 na walichumbiana yapata miaka mitatu iliyopita kwa lengo la kufunga ndoa na kuanzisha familia.
Binti huyo aliwataka watu wakome kusikiliza kile alichokitaja kuwa uwongo unaosambazwa na familia yake akisema kwamba hajashikiliwa na yeyote kinyume na matakwa yake.
“Mimi sio mtumwa wa kingono. Mimi sijatiwa kasumba na yeyote au kukabiliwa na madai ya uwongo uliosemwa kunihusu”, alisema mwanadada huyo katika hiyo video.
Aliwataka pia mashabiki wa Kelly waendelee kumwombea akiwa na imani kwamba taachiliwa hivi karibuni.
Familia ya Joycelyn ilisema katika mahojiano kwamba hawajawasiliana naye moja kwa moja kwa zaidi ya miaka mitatu na hawajui aliko.
Haya yanajiri siku chache baada ya Kelly kuwasilisha ombi mahakamani la kuachiliwa kutoka gerezani na kupatiwa kifungo cha nyumbani akidai maisha yake yamo hatarini.
Kulingana na wakili wake, mwanamuziki huyo alizirai na kukimbizwa hospitalini baada ya kupatiwa dawa nyingi kupita kiasi makusudi na wahudumu wa gereza.
Wakili huyo Beau Brindley, na wenzake wanataka Kelly wa umri wa miaka 58 apatiwe msamaha na Rais Donald Trump.
Anatumikia kifungo cha miaka 31 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa watu ambao aliwadhulumu kingono.