Watu zaidi ya 20 wameuawa na wengine wengi kuachwa na majeraha kufuatia shambulizi la bomu, baada ya mtu aliyekuwa amebeba bomu hiyo kujilipua katika kanisa la Mar Elias eneo la Dweila, jijini Damascus nchini Syria.
Hili ndilo shambulizi la kwanza la bomu la kujitoa mhanga kufa jijini Damascus tangu Bashar al-Assad aondolewe mamlakani kufuatia uasi wa kundi fulani la waisilamu mwezi Disemba.
Wizara ya usalama wa ndani nchini Syria ilisema kwamba mshambuliaji ambaye ni mwanachama wa kundi la waasi la Islamic State ambaye aliingia kwenye kanisa hilo, akafyatua risasi kiholela kabla ya kulipua bomu hilo.
Lakini ripoti nyingine zinaashiria kwamba sio mtu mmoja bali ni wawili walihusika katika shambulizi hilo la Jumapili.
Kundi la Islamic State limekuwa likihusika na majaribio ya mashambulizi katika makanisa tangu Assad alipoondolewa, lakini hili ndilo la kwanza kufanikishwa.
Wizara ya Afya nchini Syria ilitangaza kwamba waliojeruhiwa katika shambulizi hilo ni watu 52.
Video zilizosambazwa za eneo la tukio zilionyesha uharibifu mkubwa uliofanyika ndani ya kanisa hilo ikiwemo damu iliyotapakaa sakafuni.
Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa, ambaye aliongoza maasi dhidi ya Assad kabla ya kuchukua wadhifa huo kwa muda, amekuwa akisema kwamba atalinda makundi ya wachache nchini humo.