Mwanamuziki wa Tanzania Rajabu Adbul Kahali maarufu kama Harmonize ametangaza kwamba atawania ubunge wa eneo alikozaliwa la Tandahimba katika mkoa wa Mtwara, nchini Tanzania.
Harmonize alitumia Insta Stories kuwasilisha ujumbe huo ambapo alichapisha video ya Oktoba 19, 2019 ya aliyekuwa Rais Hayati John Pombe Magufuli akimsifia huku akisema kwamba anatamani awanie ubunge wa eneo alikozaliwa.
Mwanamuziki huyo aliwahi kumwimbia Magufuli wimbo mzuri yapata miaka mitano iliyopita akisifia kazi zake kama kiongozi wa nchi, wakati huo akitafuta kuchaguliwa kwa muhula wa pili.
Wimbo huo unaaminika kumgusa sana Magufuli kiasi cha kupendekeza kwamba Rajabu awanie ubunge nyumbani kwao.
Katika video hiyo Magufuli anasema, “Lakini nampongeza sana Harmonize sijui anatoka Jimbo gani? Tandahimba? Mbunge wa kule ni nani? aah ningetamani sana Harmonize aende akagombee kule awe Mbunge wa Tandahimba”.
Chini ya video hiyo ambayo amechapisha leo, Harmonize ameandika kwamba sasa yuko tayari kwa jukumu hilo la uongozi iwapo chama tawala anachounga mkono cha CCM kitaridhia.
“Sasa niko tayari kuwa mbunge wa Tandahimba kwa maslahi mapana ya Tandahimba” aliandika mwanamuziki huyo huku akimuenzi Magufuli na kumhakikishia kwamba Rais Samia ametekeleza mipango waliyokuwa nayo.
Katika chapisho lililofuata, Harmonize aliweka picha yake ya pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan na kaundika kwamba anatamani sana siku ambayo kiongozi huyo atampa fursa ya kujadili naye kuhusu maslahi ya Tandahimba.
“Naisubiri kwa hamu siku utakayonipa nafasi ya kukaa chini na kuijadili vizuri Tandahimba” aliandika Harmonize huku akidhihirisha imani kwamba Rais Samia ataibuka mshindi wa uchaguzi wa Urais wa Oktoba mwaka huu.