Mageuzi katika sekta ya kilimo yamezaa matunda, asema Rais Ruto

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto ahudhuria hafla ya 10 ya siku ya wakulima wa maziwa ya mwaka huu katika uwanja wa maonesho ya kilimo, Meru.

Rais William Ruto amesema mageuzi katika sekta ya kilimo yanaendelea kuzaa matunda, huku uzalishaji ukiimarika na wakulima wakipata mapato ya kumezewa mate.

Akizungumza wakati wa hafla ya 10 ya siku ya wakulima wa maziwa ya mwaka huu katika uwanja wa maonesho ya kilimo kaunti ya Meru, Rais alitoa mfano na sekta ya maziwa ambapo alidokeza kuwa bei ya lita moja ya maziwa imeongezeka kutoka shilingi 35 kwa lita hadi shilingi 50.

Alisema mapato ya maziwa hapa nchini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 40 hadi shilingi bilioni 59, hii ikiwa ishara kuwa sekta hiyo inazidi kuimarika.

“Ili kuendelea kuwasaidia wakulima, tumechukua hatua madhubuti za kupunguza bei ya mbegu za mifugo hadi shilingi 1,000, kunawachanja mifugo kote nchini, tumeondoa ushuru kwa mahindi ya manjano na kuhakikisha wakulima wengi wanapata vifaa vya kuhifadhi maziwa,’ alisema Rais Ruto.

Aidha aliongeza kuwa kupungua kwa bei za pembejeo za kilimo, ikiwemo mbolea, kumewawezesha wakulima kuzalisha vyakula vya kutosha humu nchini akisisitiza kuwa, serikali itaendelea kuwasaidia wakulima na kutekeleza hatua zinazoongeza uzalishaji na mapato.

Kiongozi wa taifa alisema serikali imepunguza bei ya mbolea, ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa vyakula.

Kuhusu chanjo za mifugo, Rais aliwahimiza wakulima wa Meru kuzingatia mpango wa kitaifa wa chanjo za mifugo.

TAGGED:
Share This Article