Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru, amesambaza mitungi 5,800 ya gesi ya kupikia bila malipo kwa wakazi wa eneo hilo, kama njia moja ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi.
Hatua hiyo ya Waiguru itasababisha wakazi hao kuhama kutoka utumizi wa kuni na makaa hadi kwa utumizi wa kawi safi.
Akiwakabidhi wakazi mitungi hiyo ya gesi siku ya Alhamisi, Waiguru alisema mpango huo ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuhifadhi mazingira, kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi na kuimarisha maisha kupitia mpango wa kufadhili Mabadiliko ya Tabia Nchi (FLLoCA).
Aidha, Gavana huyo alisema kuwa, serikali yake haishughulikii tu changamoto za Mabadiliko ya Tabia Nchi, lakini pia kutoa suluhu la kudumu la kukabiliana na changamoto hizo.
“Mabadiliko ya Tabia Nchi husababisha changamoto kuu kwa jamii, lakini tunachukua hatua za kijasiri kuwapa uwezo watu wetu kuimarisha ukuaji endelevu,” alisema Waiguru.
Alidokeza kuwa gesi hizo za kupikia zitasababisha kawi safi na kupunguza ukataji wa miti, na kupiga jeki afya bora kwa kupunguza uchafuzi wa hewa.
“Kwa kutumia kawi safi kupikia, tunaokoa zaidi ya miti 500 ambayo imekomaa kila mwaka na kuwapunguzia kina mama na watoto moshi ambao huhatarisha maisha yao,” aliongeza Gavana Waiguru.