Mahakama Kuu imetupilia mbali kesi iliyowalishwa na Athanas Wafula Wamunyinyi kupinga ukodeshaji wa kampuni ya sukari ya Nzoia kwa kampuni ya sukari ya West Kenya Sugar, inayomilikiwa na kampuni ya Rai kwa kitita cha shilingi bilioni 5.76.
Kupitia uamuzi uliotolewa kwa njia ya dijitali na Justice Lawrence N. Mugambi, Mahakama hiyo ilisema kesi ya Wanyonyi iliyodai kuwa umma haukuhusishwa kwenye mchakato huo, ilikuwa imetatuliwa kwenye kesi kati ya Martin Nyongesa Barasa na Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo na wengine (Kesi nambari. E065 ya 2024).
Kampuni ya sukari ya West Kenya, ilipata idhini ya kusimamia shughuli za kampuni ya sukari ya Nzoia chini ya mpango mpana wa kufufua sekta ya sukari hapa nchini.
Awali waziri wa kilimo Mutahi Kagwe alipongeza utendakazi wa kampouni ya sukari ya West Kenya, kutokana na sera zake alizotaja zinawafaidi pakubwa wakulima wa miwa.
Siku ya Alhamisi, serikali ilitoa shilingi milioni 200 kulipa deni la mishahara ya wafanyakazi wa kampuni ya sukari ya Nzoia, na kufikisha shilingi milioni 800 ambazo tayari zimetolewa na serikali kulipa mishahara ya wafanyakazi wa kampuni hilo.