Linc na Yul Edochie waonyeshana mapenzi mitandaoni

Ndugu hao wametumia kauli ya damu kuwa nzito kuliko maji huku wakisifiana na kuonyeshana mapenzi.

Marion Bosire
2 Min Read

Kaka wawili Yul na Linc Edochie wameonyeshana mapenzi katika mitandao ya kijamii, hali ambayo imefurahisha mashabiki wa waigizaji hao wa Nollywood.

Wana hao wa mwigizaji mkongwe Pete Edochie wamewahi kutofautiana hadharani awali na tukio la hivi punde lilianzishwa na Linc ambaye aliamua kumsifia mdogo wake Yul kupitia chapisho mitandaoni.

Linc alichapisha video inayomwonyesha yeye na Yul wakikumbatiana kwa furaha na kumiminiana sida kisha akaandika, “Damu ni nzito kuliko maji. Wengi hawajui hili, ni kakangu Yul aliniomba nirejelee uigizaji mwaka 2015 baada ya kuususia kwa muda”.

Aliendelea kuelezea kwamba kila mara alikuwa anaahirisha urejeo wake katika tasnia ya filamu hadi mwaka 2020 alipoamua na kuingilia fani hiyo ambayo pia ni ya baba yao mzazi.

Kulingana na Linc, Yul ndiye alimgunza mbinu mbali mbali za uigizaji kwa sababu amesomea kazi hiyo na yeye ni kuipenda tu.

“Umpende usimpende huyu jamaa anasalia kuwa mmoja wa waigizaji wakuu na waandalizi wa filamu humu nchini” alimalizia Linc huku akimtakia Yul baraka za mwenyezi Mungu.

Yul naye amejibu ujumbe wa kakake mkubwa ambapo alikubaliana naye kwamba damu ni nzito kuliko maji huku akimhakikishia kwamba atasimama naye milele na kumtakia baraka za Mungu.

Wadadisi mitandaoni wanahisi kwamba wawili hao wameungana dhidi ya mke wa kwanza wa Yul aitwaye May ikikumbukwa kwamba punde baada ya Yul kutambulisha mke wake wa pili Judy Austin, Linc alichagua kusimama na May wazi wazi.

Lakini baada yake kuachana na mke wake wa kwanza na kuoa mke mwingine, Linc sasa amemsaaza May na anaunga mkono kakake Yul.

Share This Article