Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta, KNH imetoa taarifa kuhusu waliojeruhiwa katika maandamano ya jana na kupelekwa huko kwa matibabu.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. William Sigilai ilianza kwa maelezo kuhusu jamaa aliyeonekana kwenye video akipigwa risasi na polisi jijini Nairobi.
Mwanamume huyo ambaye alikuwa akiuza barakoa alifikishwa KNH saa tisa na dakika 16 alasiri akiwa na jeraha la risasi na alipofanyiwa uchunguzi, risasi hiyo ilionekana ikiwa ndani ya kichwa chake, upande wa kulia.
Alipelekwa kwenye chumba cha upasuaji saa tatu kasoro dakika kumi ambapo risasi hiyo ilitolewa kisha akalazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo anaendelea kupata huduma.
“Huku hali yake ikiwa mbaya, bado yuko hai na yuko chini ya uangalizi na utunzaji wa kila mara kutoka kwa wahudumu wetu,” ilielezea taarifa hiyo.
DKT. Sigilai alielezea pia kwamba walipokea jumla ya majeruhi 16 kutokana na maandamano ya jana, waliokuwa na majeraha ya risasi na ya kupigwa na vifaa butu.
Saba kati yao bado wamelazwa hospitalini humo kwa huduma zaidi, tisa walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka, wawili wamefanyiwa upasuaji na wanne walikuwa wafanyiwe upasuaji leo.