Tyler Perry ashtakiwa kwa dhuluma za kingono

Ameshtakiwa na mwigizaji wa kipindi chake cha "The Oval" aitwaye Derek Dixon.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji na mwandalizi maarufu wa filamu nchini Marekani Tyler Perry, ameshtakiwa kwa kile kinachosemekana kuwa dhuluma za kingono dhidi ya mwigizaji aliyehusika kwenye kipindi chake.

Mwigizaji huyo kwa jina Derek Dixon, amewasilisha kesi mahakamani akitaka alipwe fidia ya Dola milioni 260 na Perry.

Derek Dixon ambaye aliigiza kama Dale katika kipindi cha runinga kiitwacho “The Oval” cha Tuler Perry, anadai kwamba Perry alimdhulumu vibaya kingono, akamshambulia na hata kumpiga pamoja na kumdhalilisha kikazi alipokosa kukubali kuhusiana naye.

Wakili wa Perry aitwaye Matthew Boyd ametaja madai ya Dixon kuwa kashfa tu ambayo haitamtikisa mteja wake na wanaamini kwamba yatathibitishwa kuwa ya uwongo.

Kwenye stakabadhi za kesi hiyo iliyowasilishwa Ijumaa katika mahakama moja ya Los Angeles, Dixon anaelezea kwamba alikutana na Perry mwaka 2019 alipokuwa akifanya kazi kwenye kampuni moja ya maandalizi ya hafla ambayo ilikuwa imeandalia Perry sherehe.

Hapo ndipo walibadilishana nambari za simu na wakawasiliana baadaye kuhusu kubadili taaluma na kuwa mwigizaji. Anasema baada ya hapo, Perry alianza kumtumia jumbe za kingono zilizojumuisha picha. b

Kulingana na Dixon, mwaka 2020 Perry alimwalika nyumbani kwake huko Douglasville, Ga karibu na Atlanta ambapo walijifurahisha kwa vinywaji kisha akaenda kulala katika chumba cha wageni.

Anaelezea kwamba Perry alijiunga naye kitandani akaanza kumpapasa akaruka kutoka huko kisha akamfahamisha mwenyeji wake kwamba hangependelea kushiriki ngono naye.

Dixon anasema kwa muda mrefu alisusia jumbe za Perry hadi wakati alimpa fursa ya kuigiza kwenye kipindi cha The Oval.

Share This Article