Familia ya Joycelyn Savage yapinga msamaha wa R. Kelly

Mchumba huyo wa R. Kelly wa umri wa miaka 24 hajawasiliana na familia yake kwa muda wa miaka minne.

Marion Bosire
2 Min Read
Joycelyn Savage

Familia ya mwanamke aitwaye Joycelyn Savage wa miaka 24, ambaye alikuwa mchumba wa mwanamuziki R. Kelly imepinga hatua ya kumpa mwanamuziki huyo anayezuiliwa msamaha.

Wanaamini kwamba binti yao Joycelyn ambaye hawajui aliko tangu mwaka 2019 ni mmoja wa wahasiriwa wa Kelly na ambaye wanaamini hadi sasa yuko chini ya udhibiti wake.

Wakili wa familia hiyo aitwaye Gerald Griggs naye pia ameshikilia msimamo wa wateja wake kuhusu mwanao ambaye waliongea naye mwisho kwa njia ya simu mwaka 2019 na tangu wakati huo anawasiliana nao kupitia kwa watu wengine.

Hata hivyo wanaamini yuko hai, buheri wa afya na wangependa sana kuwasiliana naye moja kwa moja.

Wanataka Kelly wa umri wa miaka 58, ambaye kupitia kwa mawakili wake anatafuta msamaha kutoka kwa Rais Trump, atumikie kifungo chake chote cha miaka 31.

Mwaka 2021, Kelly alihukumiwa na mahakama ya New York, kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa watu ambao aliwadhulumu kingono.

Mwaka mmoja baadaye alikabiliwa na kesi nyingine ambapo alipatikana na hatia kuhusiana na makosa ya kutumia watoto kingono na kunakili picha zao za kingono na makosa ya kushawishi watoto kushiriki ngono naye huko Illinois.

Wakili wa Kelly, Beau Brindley, amekataa kuangazia suala la Joycelyn kwa sasa akisema wanachopigania sasa ni kupata angalau kifungo cha nyumbani kwa mteja wake ambaye anadai maisha yake yako hatarini gerezani.

Hii ni baada yake kudai kupatiwa dawa kupita kiasi makusudi na kuzidiwa kiasi cha kulazwa hospitalini.

Share This Article