Kenya na China zimekubaliana kuimarisha na kupanua ushirikiano katika sayansi, utafiti, uvumbuzi na teknolojia ili kuchochea mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika nchi hizo mbili.
Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba ameitaja hatua hiyo kuwa muhimu kwani inawiana na Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA) ya serikali ya Kenya Kwanza na Maono ya mwaka 2030.
“Kenya na China zimejenga uhusiano thabiti wa pande mbili, hasa katika elimu, utafiti, sayansi, teknolojia na uvumbuzi,” alisema Waziri Ogamba wakati akihudhuria Mkutano wa Pili wa Mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja juu ya Mabadilishano ya Sayansi na Teknolojia mjini Chengdu nchini China.
“Uhusiano huu umekuwa wenye manufaa kwa nchi zote mbili, ukihamasisha ushirikiano, kukuza uwezo, na maendeleo ya teknolojia.”
Wakati akiwa nchini China, Waziri Ogamba alishiriki mkutano na Waziri wa Sayansi na Tekolojia wa China, Yin Hejun.

Wawili hao walikubaliana kuimarisha na kupanua ushirikiano katika sayansi, utafiti, uvumbuzi na teknolojia hususan kwa kutumia Makubaliano juu ya
Ushirikiano wa Kisayansi na Teknolojia yaliyotiwa saini na nchi hizo mbili.
Ili kuongoza utekelezaji wa makubaliano hayo, Mawaziri hao walitia saini Barua ya Dhamira inayoainisha nyanja muhimu za ushirikiano.
