Mwanamuziki wa Tanzania Naftal Mlawa maarufu kama Nuh Mziwanda anaonekana kuwa na imani kwamba nyota yake ya mafanikio ipo mikononi mwa mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz.
Msanii huyo wa Bongo Fleva amekuwa akitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii hususan Instagram kumwomba Diamond Platnumz ushirikiano wa kikazi almaarufu colabo ili aweze kuinuka kimuziki.
Diamond amegonga vichwa vya habari hivi karibuni baada ya tamasha lake la London kufanikiwa ambapo Mziwanda mwenyewe alishangaa akisema, “Diamond alivyojaza show yake London kweli naweza kupata collabo?”
Aliambatanisha ujumbe huo na maneno ya kumpongeza akisema watanzania wanajivunia ufanisi wake na kuongeza kwamba, “Kila msanii anataka hayo. Sisi tunajuana bwana unayofanya ndio ndoto zetu”.
Katika chapisho jingine alisema, “Niokoe ndugu. Nipo gheto tumepishana miaka michache sana angalia jumbe zako,” akimlenga Diamond huku akimwomba waingie naye studio.
“Naomba uamue tufanye studio session” alisema akimwomba ampe riziki hata ingawa anajua kwamba anayetoa ni Mungu.
Mziwanda amemhusisha pia mamake Diamond ambaye alichapisha picha yake na kuandika, “Mama ongea na Mwanao anisaidie nakuomba Mama yangu. Muziki una mengi please Mama yangu Mwambie Naseeb anifungulie Njia Mpya”.
Baba Levo ambaye ni mtu wa karibu wa Diamond Platnumz alitoa maoni yake kwenye chapisho hilo la Mziwanda akisema, “Diamond Platnumz hawezi kufanya kazi na TEJA” isijulikane alikuwa anamaanisha nini.
Kando na Diamond, msanii huyo ambaye umaarufu wake ulionekana kubuma kwa muda amewaomba pia wasanii kama vile Rayvanny, Marioo na Jay Melody collabo.
Hata hivyo, ujumbe wake kwa Wasanii hao huenda hakupata majibu kutokana na picha za mawasiliano alizochapisha zinazoonyesha maandishi yake pekee.
Nuh Mziwanda ni mmoja kati ya Wasanii waliofanya vizuri awali hasa wakati alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Shilole ambapo alitoa nyimbo kama ‘Jike shuka’.