Mshukiwa wa mauaji ya kiongozi mmoja na majaribio ya kuua wa pili huko Minnesota, nchini Marekani amekamatwa. Vance Boelter wa umri wa miaka 57 alikamatwa Jumapili baada ya msako wa siku mbili.
Afisi ya mkuu wa sheria katika jimbo la Ramsey ilielezea katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii kwamba mshukiwa amekamatwa huku ikichapisha picha yake.
Katika chapisho hilo, afisi ya mkuu huyo wa sheria ilishukuru maafisa wote wa vitengo mbali mbali vya sheria na raia waliojitolea kusaka mtu huyo ikisema sasa haki itapatikana.
Boelter aliwapiga risasi viongozi wawili wa chama cha Democratic na wanandoa wao katika makazi yao katika kile kinachoaminika kuwa shambulizi lililochochewa na siasa.
Melissa Hortman mwakilishi wa Minnesota na mume wake Mark walifariki katika shambulizi hilo huku seneta John A Hoffman na mke wake Yvette wakiachwa na majeraha.
Boelter ambaye anajihusisha na masuala ya huduma za usalama ambaye aliwahi kuhudumu kwenye bodi moja ya ukuzaji wa wafanyakazi na Hoffman, sasa atakabiliwa na masktaka mawili ya mauaji na mawili ya kujaribu kuua.
Gavana wa Minnesota Tim Walz alipongeza maafisa wa usalama kwa kukamata mshukiwa akisema, walikimbia kuelekea maeneo yasiyo salama kuhudumia jimbo la Minnesota.
Huku akitoa rambi rambi zake kwa jamaa za Hortman, Walz alielezea kwamba Hoffman na mkewe wanaendelea kupata nafuu.