Mwanamuziki maarufu kutoka Uganda, Bebe Cool, anathibitisha kuwa umri ni nambari tu huku akiendelea kutawala tasnia ya muziki akiwa na miaka ya 40 na zaidi.
Msanii huyu wa umri wa miaka 47, hivi karibuni alifunguka kuhusu anavyofanikiwa kubakia muhimu, mwenye nguvu na kuendelea kushawishi vijana kupitia muziki, hata baada ya zaidi ya miongo miwili katika tasnia hiyo.
Akiwa ametoka tu kuzindua albamu yake mpya iitwayo ‘Break the Chains’ Bebe Cool alitafakari changamoto za kuzeeka katika ulimwengu wa muziki unaobadilika kwa kasi.
“Hakuna mtu anayetaka kuzeeka; unataka kukua lakini sio kuzeeka,” alisema.
Anasema siri ya kuendelea kung’aa ni mbinu yenye mizani, amejizingira na watu wa kizazi chake walio na uzoefu, pamoja na timu changa ya vijana wabunifu.
Mchanganyiko huo, anasema, hufanya muziki wake ubakie na mizizi na kuwa wa kisasa.
Bebe Cool pia ameamua kuvunja matarajio ya jamii kuhusu taswira ya kuzeeka. “Niliamua sitakuwa yule mzee wa kuvaa suti na tai” alisema. “Kimwili, nimekataa kuzeeka.”
Yeye huutunza mwili wake kwa mazoezi ya kawaida ya viungo, akisisitiza kuwa afya ya mwili ni muhimu kwa kudumisha mwonekano wa ujana. “Ukiachilia mwili, haijalishi utakavyovaa au kujitahidi kuonekana wa kisasa, uzee utaonekana tu,” alieleza.
Alitambua ushawishi wa vijana katika maeneo ya kitamaduni na kiuchumi siku hizi akiongeza kwamba amekuwa makini kujibadilisha ili kuendana na mtindo wao.
“Serikali na kampuni kubwa sasa zinawalenga vijana. Kwa hiyo, unawalengaje? Lazima uwe kama wao, ufikiri kama wao, uonekane kama wao,” alibainisha.
Kwa kuukumbatia mabadiliko, kubaki mwenye afya na kufikiri kijana, Bebe Cool anaendelea kuimarisha urithi wake kama gwiji katika muziki wa Uganda.