Mbunge auwawa Marekani, polisi watafuta mshukiwa

Seneta Tim Walz anaamini kwamba mashambulizi dhidi ya kiongozi huyo yalichochewa na siasa.

Marion Bosire
2 Min Read
Melissa na Mark Hortman

Mbunge wa chama cha Democratic na mume wake walipigwa risasi na kuuawa nyumbani kwao Jumamosi asubuhi katika kile kinachoaminika kuwa mauaji yaliyochochewa na siasa.

Melissa Hortman wa umri wa miaka 55 ambaye ni mwakilishi wa Minnesota na mume wake Mark Hortman walikabiliwa na mshukiwa wakiwa nyumbani kwao katika eneo la Brooklyn Park, mji ulio karibu na Minneapolis nchini Marekani.

Seneta John Hoffman wa umri wa miaka 60 ambaye pia ni mwanachama wa chama cha Democratic na mkewe walilengwa na mshukiwa huyo katika makazi yao yaliyo karibu.

Walipigwa risasi mara kadhaa lakini wanaripotiwa kuendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji kulingana na Seneta Tim Walz ambaye anasema wana matumaini japo ya tahadhari kwamba wawili hao watapona.

Maafisa wa usalama tayari wameanzisha uchunguzi wa kuwezesha kukamatwa kwa mshukiwa wa visa hivyo ambaye alijisingizia kuwa afisa wa polisi.

Jina la Seneta Tina Smith mwakilishi wa Minnesota huko Washington lilikuwa kwenye orodha ya majina iliyopatikana kwenye gari linalohusishwa na mshukiwa wa mauaji ya Hortman na mume wake.

Kulingana na afisi yake iliyowasiliana na shirika la BBC kwa njia ya barua pepe, yeye pia alikuwa analengwa na mshukiwa.

Shirika la FBI limetangaza zawadi ya Dola elfu 50 kwa yeyote aliye na habari zinazoweza kusaidia katika kukamata mshukiwa ambaye ametambuliwa kama Vance Luther Boelter.

Share This Article