Waendeshaji magari watagharamika zaidi zaidi baada ya mamlaka ya kudhibiti kawi na bidhaa za petroli (EPRA), kuongeza bei ya mafuta ya petroli kwa shilingi 2 na senti 69 kwa kila lita.
Kwenye taarifa ya EPRA bei mpya ya bidhaa za mafuta ya petroli itakuwa shilingi 177 na senti 42 kwa kila lita moja kuanzia leo hadi Julai 14 mwaka huu.
Hata hivyo afueni ni kuwa bei ya mafuta taa na dizeli imepunguzwa ,ambapo dizeli imepunguzwa kwa shilingi 1 na senti 95 ,huku mafuta taa yakipunguzwa bei kwa shilingi 2 na senti 69 kwa kila lita.
Dizeli sasa itauzwa kwa shilingi 162.91, kwa kila lita huku bei mpya ya mafuta taa ikiwa shilingi 146.93, kwa kila lita moja.