Serikali imetenga rasilimali za kutosha kufufua na kukamilisha ujenzi wa barabara kote nchini, huku ikianzisha ujenzi wa barabara mpya kufanikisha shughuli za uchukuzi wa watu na bidhaa.
Akizungumza katika kaunti ya Nyamira, Naibu Rais Kithure Kindiki alisema ujenzi wa barabara nane kwenye kaunti hiyo tayari unatekelezwa, ikiwemo ile ya kilomita 61 ya Eronge -Kebuse- Kahawa Border-Borabu-Omonyenye-Amakara–Isonge-Chebilati-Chericha-Simba Uti-Tinderet kwa kima cha shilingi bilioni 3.6.
Aidha alisema kititta cha shilingi milioni 519, kimetengwa kwa mradi wa uunganishaji umeme wa Last Mile katika kaunti hiyo ya Nyamira, ambapo nyumba 7,500 zitanufaika.
Na kuhusu ujenzi wa soko za kisasa, Kindiki alisema masoko ya Miruga, Ekonga na Nyamaya yatejengwa kufanikisha biashara ya vyakula katika eneo hilo.
Alidokeza kuwa nyumba za malazi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Taasisi za Kiufundi pia zitajengwa ili kuwapa wanafunzi mazingira bora ya masomo, kupata ujuzi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa hili.