Rais William Ruto ametoa ahadi ya kuwalinda wakenya dhidi ya maafisa wa polisi wakatili, huku akiwaonya maafisa hao kuwa watawajibikia matendo yao.
Kiongozi wa taifa aliyasema hayo leo Ijumaa katika Chuo cha Uongozi cha Huduma ya Taifa ya Polisi kilicho Ngong, kaunti ya Kajiado, alipokuwa akiongoza hafla ya kuharibu zaidi ya bunduki 6,000 haramu zilizonaswa kati ya mwaka 2022 na 2025.
“Pia tumejitolea kuwalinda wakenya dhidi ya maafisa wa polisi wakatili. Maafisa wa polisi ambao ni wahalifu watachukuliwa hatua,” alisema Rais Ruto.
Matamshi yake yanajiri siku kadhaa baada ya kifo cha mwanablogu Albert Ojwang’, kilichotokea katika kituo cha polisi cha Central Jijini Nairobi, katika hali ya kutatanisha, hatua iliyosababisha maandamano Nairobi.
Wakati huo huo, kiongozi wa nchi aliwapongeza wakenya ambao walisalimisha kwa hiari bunduki walizokuwa wakimiliki kwa njia haramu kupitia mpango wa kijamii wa kutwaa silaha haramu.
“Uharibifu wa silaha hizi unaashiria lengo kuu la kukabiliana na utovu wa usalama. Nawapongeza maafisa wa usalama na wananchi wakiwemo viongozi wa dini, wale wa kijamii ambao wamefanikisha hatua hii,” alisema Rais Ruto.
Aidha aliagiza asasi zote za usalama kutumia vyema silaha na kuhakikisha usimamizi na udhibiti bora wa silaha zilizo chini yao.