Uganda yakanusha madai ya kuzuka tena kwa Covid 19

Serikali imechukua hatua hiyo kufuatia ripoti kwamba maradhi hayo ya Covid 19 yamerejea nchini humo.

Marion Bosire
2 Min Read

Wizara ya Afya ya Uganda imekanusha madai ya kuzuka upya kwa maradhi ya Covid 19 nchini humo, kufuatia ripoti zilizoenezwa hivi karibuni kwamba ugonjwa huo umezuka tena.

Kulingana na wizara hiyo, picha na video zinazosambazwa mitandaoni ni za matukio ya zamani na zinasambazwa na watu ambao wanataka kupotosha umma.

Mkurugenzi mkuu wa huduma za Afya Daktari Charles Olaro, amehakikishia raia wa Tanzania kwamba Covid 19 haijarejea tena nchini Uganda.

“Hali ya kitaifa imeendelea kuwa tulivu na chini ya udhibiti kamili tangu kumalizika kwa mlipuko mkubwa wa COVID-19 miaka mitatu iliyopita” alisema Dkt. Olaro.

Wizara ya Afya imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali hiyo na kuhakikisha utambuzi wa mapema na mwitikio wa haraka kwa vitisho vyovyote vya kiafya.

Inaendelea kufuatilia aina mpya za virusi zinazoripotiwa kote duniani na inashirikiana na wadau husika ili kuhakikisha usalama wa umma.

Olaro alisema Uganda ina mfumo imara wa ufuatiliaji na mwitikio, ambao unaendelea kufanya kazi kikamilifu na una uwezo wa kukabiliana na vitisho vyovyote vya kiafya vinavyoweza kutokea.

Wizara hiyo imeshauri kwamba mtu yeyote anayeonyesha dalili za COVID-19 atembelee kituo cha afya kilicho karibu ili apate matibabu yanayofaa.

Pia imehimiza umma kuendelea kufuata taratibu nzuri za usafi kama kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi na sabuni au kutumia kisafishaji chenye pombe.

Share This Article