Mwanamuziki wa Tanzania Billnass ameibuka na ushauri kwa vijana wenye talanta katika tasnia mbali mbali zinazohusisha umaarufu kama vile muziki na uigizaji.
Msanii huyo alitumia Insta Stories kutoa ujumbe huo ambapo aliandika, “Kwa vijana wote, wadogo zangu na rafiki zangu mliobarikiwa na vipaji mbali mbali, kabla ya kuingia kwenye tasnia yoyote inayohusiana na Umaarufu Tanzania !! Muombe sana Mungu akupe nguvu ya uvumilivu na roho ya kustahimili!”
Kulingana naye tasnia zinazohusisha umaarufu zimejaa vita vya kila aina, usaliti, ushetani na dhuluma. “kuanzia kwa wadau, mameneja, kampuni za usambazaji, kampuni za muziki na kadhalika” alisema.
Billnass aliwashauri vijana wenye talanta akisema kwamba sio rahisi kutajirika kutokana na kazi kama hizo lakini ni rahisi kuingia pabaya kama kwenye msongo wa mawazo na hata kuingilia uraibu wa mihadarati.
“Swala la kutajirika ama kupata pesa kupitia hizi kazi sio rahisi kama unavyoskia ila Kupata msongo wa mawazo, kupoteza maisha, kupata maradhi, kuchanganyikiwa ama Kuingia Kwenye uraibu ni rahisi kuliko kutengeneza pesa.” aliandika msanii huyo.
Aliendelea kuwasisitizia kwamba wawe makini sana na waingilie tasnia hizo wakiwa tayari na wamtangulize Mungu akisema, “Unaweza Kupambana ili uisaidie familia yako kumbe ndio unaenda Kuleta janga ambalo familia yako itakuwa kwenye jukumu la Kuteseka kukusaidia”.
Ushauri huu wa Billnass unajiri wakati ambapo anaendeleza tamasha lake linalolenga vijana kwenye taasisi za elimu ya juu ambalo amelipa jina la “Chuo kwa chuo”.
Wakati alitangaza ujio wa tamasha hilo Billnass alifafanua kwamba litahusisha burudani pamoja na ushauri faafu kwa wanachuo.