Vijana kote nchini wamehimizwa wajiunge na taasisi za mafunzo ya kiufundi kama njia ya kujipatia ujuzi utakaowahakikishia ajira ya kudumu maishani.
Wito huu ulitolewa na katibu wa elimu ya kiufundi katika wizara ya elimu Esther Thaara Muoria katika mahojiano na msemaji wa serikali Isaac Mwaura kwenye kipindi Sema na Spokes Bonga na Gava.
“Mara tu unapopata ujuzi huwezi kulala njaa. Unaweza kuanzisha biashara yako mwenyewe, unaweza kuajiriwa nchini, katika kanda hii au kimataifa” alisema Esther katika mahojiano hayo.
Muoria alifichua kwamba serikali ya Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais William Ruto ilibuni mpango wa kuhakikisha kwamba kila eneo bunge nchini linapata taasisi ya mafunzo ya kiufundi, hatua ambayo kulingana naye inaendelea kutekelezwa.
Alisema kufikia sasa taasisi hizo ni 240 kumaanisha kwamba ni maeneo bunge yapatayo 50 pekee ambayo hayajapata vituo vya mafunzo ya kiufundi.
Katika kuorodhesha mafanikio ya idara ya elimu ya kiufundi, Katibu Muoria alisema kwamba mfumo wa mafunzo ulibadilika kabisa katika taasisi hizo kwani sasa wanaangazia mafunzo ya kivitendo sana na wala sio nadharia tu.
Alitaja pia kwamba wanatumia mfumo wa Ujerumani wa mafunzo ambapo wanafunzi wanapata asilimia 50 ya mafunzo katika taasisi zao na nyingine 50 katika maeneo ya kazi au viwandani.
Muoria alitania kwamba mfumo huo umesababisha tatizo chanya ambapo wanafunzi mara nyingi hawarejei darasani kufanya mtihani wa mwisho kwani wameshapata ajira nyanjani.
Fanikio jingine la idara ya elimu ya kiufundi kulingana na Katibu Muoria ni kupitishwa kwa sera ya utambuzi wa ujuzi wa awali na kuundwa kwa kurugenzi spesheli katika taasisi ya mafunzo ya kiufundi ya Kabete kuhakikisha utekelezaji wa sera hiyo.
Kutokana na hilo, wajuzi wapatao 2700 wamepatiwa mafunzo katika taasisi ya Kabete na watatumika kutathmini ujuzi wa awali wa watu.
Utathmini huo kulingana naye, utatekelezwa katika namna itakayofaa kila mmoja bila vizingiti kama vile lugha rasmi.