Timu ya soka ya shule ya upili ya wavulana ya Kakamega almaarumu “Green Commandoes” imefuzu hii leo jumanne kwa mashindano ya kaunti ya Kakamega kufuatia ushindi wa magoli tano kwa moja dhidi ya shule ya Shieywe kwenye finali ya kaunti ndogo ya Lurambi iliyosakatwa katika uga marufu wa shule ya Kakamega – Mabao stadium.
Awali, mchuano huo uliratibiwa kukaragazwa wikiendi iliyopita ila ukahairishwa kufuatia marudio ya robo fainali baina ya Kakamega na majirani wao Kakamega Town ship kule chuoni sigalagala ambapo Kakamega ilishinda kwa magoli matatu kwa nunge.
Baada ya ushindi huo, timu hiyo itaanza kusaka taji la kaunti tarehe 18 mwezi huu katika shule ya St. Peters Mumias itakapomenyana na Munyuki (Lugari) na Mwihila (Kwisero) katika kundi B.
Zingine zinazosaka taji hilo ni wenyeji St.Peters, mabingwa watetezi Musingu (ikolomani) St. Mathias Mwitoti na St. Maurice Mwira zote za kundi A.
Kwenye kundi C, ni Butere, St. Bonface Mapera, Ingotse (Navakholo) na mabingwa wa mkoa magharibi mwaka wa 2023 – Shanderema (shinyalu).
Lugusi, St. Michael Ingusi na Holy Family Marakusi zinafunga kundi la mwisho la D.
Shule zitakazo tinga fainali zitawakilisha kaunti hiyo kwenye mashindano ya eneo la magharibi mwezi ujao katika shule hiyo ya Kakamega.