Maafisa wa kituo cha Central wasimamishwa kazi

Hatua hii inatokana na kifo cha kutatanisha cha Albert Ojwang katika seli za kituo hicho cha polisi cha Central Jumamosi usiku.

Marion Bosire
2 Min Read

Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja ameamuru kusimamishwa kazi kwa afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi na polisi waliokuwa zamu humo Jumamosi usiku.

Kanja amechukua hatua hii kufuatia kifo cha kutatanisha cha Albert Ojwang katika kituo hicho cha polisi cha Central, Nairobi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo alfajiri, huduma ya taifa ya polisi NPS ilifahamisha umma kwamba kusimamishwa kazi kwa maafisa hao wa polisi kunalenga kutoa fursa ya uchunguzi wa kina, usio na upendeleo na wa haraka.

Uchunguzi huo utaendeshwa na mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi nchini IPOA.

“Inspekta Jenerali wa polisi ameamuru kusimamishwa kazi mara moja kwa maafisa wafuatao 1. Afisa mkuu wa kituo (OCS) kituo cha polisi cha Central, 2. Afisa mkuu wa zamu wa siku husika, 3. Afisa msimamizi wa seli wakati huo, 4. maafisa wa zamu katika afisi ya ripoti usiku huo na 5. Afisa yeyote aliyehusika na kitendo hicho” ilisema taarifa hiyo.

Kifo cha kutatanisha cha Albert Ojwang kimezua lalama si haba kutoka kwa wakenya hasa kwa mitandao ya kijamii.

Ojwang ambaye alikuwa mwalimu, mtoto wa pekee wa kiume wa babake na mzazi wa kitoto cha miezi miwiki alikamatwa Jumamosi huko Homa Bay na kusafirishwa hadi Nairobi.

Kulingana na polisi, Ojwang alikamatwa kuhusiana na chapisho la kughadhabisha katika mtandao wa X. Alizuiliwa katika kituo cha Central na Jumapili akasemekana kuwa amefariki kutokana na maumivu ya kichwa aliyojisababishia.

Share This Article