Rais William Ruto amesema kwamba amejitolea kuhakikisha mabadiliko nchini wakati wa uongozi wake. Alikuwa akizungumza jana alipohudhuria ibada katika kanisa la CCA, eneo bunge la Makadara kaunti ya Nairobi.
Huku akisisitiza kwamba ataangazia tu kuleta mabadiliko nchini, kiongozi wa nchi aligusia ufanisi wa mabadiliko katika sekta kama elimu na kilimo, mpango wa nyumba za gharama nafuu na halmashauri ya afya ya jamii SHA.
Kulingana naye, mipango hiyo inabadilisha maisha ya watu wa tabaka la chini kuambatana na mkakati wa serikali ya Kenya Kwanza wa kiuchumi Bottom Up.
Rais alisema pia kwamba serikali ya kitaifa itaendelea kushirikiana na serikali ya kaunti ya Nairobi kuboresha mwonekano wa jiji kuu huku akihimiza vijana wajisajili kwenye mpango wa Climate Works.
Baada ya ibada, Rais Ruto alizuru mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Jogoo Road Phase 1 ambapo alisifia maendeleo yake. Nyumba hizo 2,760 zitakapokamilika zinatarajiwa kuwapa wakazi makazi ya kisasa na ya hadhi.
Alielezea kwamba miradi zaidi ya 200 sawa na huo wa Jogoo Road Phase 1 inaendelea katika sehemu mbali mbali za nchi na ikikamilika vile bile, wakenya hasa wa mapato ya chini watapata makazi mazuri ya gharama nafuu.
Kiongozi wa nchi alizuru pia uwanja wa michezo wa Uhuru ambao uko katika eneo bunge la Embakasi Magharibi.