Rais wa Marekani Donald Trump amemwonya mkwasi Elon Musk ambaye alikuwa rafiki yake namfadhili wa kampeni yake dhidi ya kufadhili wawaniaji wa chama pinzani cha Democratic katika uchaguzi ujao wa katikati ya muhula mwaka 2026.
Haya yanajiri wakati ambapo uhusiano kati ya Trump na Musk unazidi kudorora huku Trump akionya kwamba iwapo atachukua hatua hiyo ataadhibiwa vikali.
Trump alisema haya katika mahojiano na kituo cha NBC News Jumamosi lakini hakutaja hatua atakazochukua dhidi ya Musk.
Wasaidizi wa Trump, watu wa chama chake cha Republican na wafadhili wamekuwa wakishauri kwamba yeye na Musk wawekekando tofauti zao na wadumishe amani, wakihofia kwamba huenda wakakosana vibaya kisiasa na hata kiuchumi.
Rais huyo alisema kwamba anaamini uhusiano kati yake na Musk umekwisha.
Musk alighadhabishwa na mswada wa Trump kuhusu ushuru na matumizi ya fedha ambao aliutaja kuwa chukizo huku akitoa habari za kushangaza kuhusu uhusiano wa Trump na marehemu Jeffrey Epstein.
Epstein alikuwa mkosaji wa kingono ambaye alikuwa na washirika wengi ambao majina yao hayajawahi kufichuliwa. Alijitoa uhai mwaka 2019 alipokuwa akikabiliwa na mashtaka hayo.
Musk hata hivyo amefuta chapisho la madai ya Trump kuwa mmoja wa washirika wa Epstein kutoka X.
Serikali ya Trump tayari imekubali kwamba inachunguza stakabadhi kadhaa, video na vitu vingine vilivyotokana na uchunguzi na kuahidi kutoa majina ya watu maarufu waliohusika katika uhalifi wa Epstein.