Kamati ya bunge la Seneti kuhusu Kilimo imeelezea wasiwasi kuhusu unyakuzi wa ardhi iliyokusudiwa kwa utafiti wa kilimo humu nchini.
Kamati hiyo imesema; shirika la utafiti wa kilimo na mifugo humu nchini (KALRO) ndilo lililoathiriwa mno huku ikibaini kuwa hali hiyo inaathiri uzalishaji na utafiti wa humu nchini.
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Bungoma David Wakoli ilionya kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaofanya kazi na maafisa wa serikali walikuwa wakilenga ardhi ya KALRO, hatua ambayo imeathiri vibaya utendakazi.
Akizungumza baada ya kuzuru kituo cha KALRO mjini Naivasha, Wakoli alipongeza taasisi hiyo kwa huduma inayotoa kwa wakulima licha ya matatizo ya kifedha.
Kwa upande wake, Seneta wa Kisumu Tom Ojienda alisema Sheria ya KALRO ya mwaka wa 2013 inafaa kufanyiwa marekebisho, ili kuwezesha taasisi hiyo kutekeleza shughuli zake.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na mwenzake wa Embu Alexander Mundigi ambaye alitaja unyakuzi wa ardhi ya KALRO kuwa tishio kuu kwa uwepo wa chakula nchini.