Rais William Ruto, leo Alhamisi alikuwa mwenyeji wa viongozi wa kaunti ya Siaya katika Ikulu ya Nairobi, ambapo aliwahakikishia viongozi hao kwamba Serikali ya Taifa itapiga jeki miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.
Rais Ruto alisema kuwa serikali ya taifa itawekeza kitita cha shilingi bilioni moja katika uchumi wa baharini, zikiwemo shilingi milioni 600 za ustawishaji wa Usenge Pier na shilingi milioni 400 za ujenzi wa soko la samaki.
Aidha, Rais alidokeza kuwa Serikali Kuu itajenga masoko 16 katika kaunti ya Siaya kwa kima cha shilingi bilioni 2.5, huku shilingi bilioni 61.6 zikitengwa kwa uunganishaji umeme wa last mile kwa nyumba 16,000.
“Tunatafuta shilingi zingine milioni 500 kuwezesha uunganishaji nyumba 5000 kwa umeme,” alisema Rais Ruto.
Kuhusu kilimo, kiongozi wa taifa alisema kaunti ya Siaya pamoja na kaunti zingine, zitanufaika na mradi wa serikali wa kilimo cha pamba, ambacho kinauwezo wa kutoa nafasi za ajira na uhakikisha mapato kwa wakulima.
Alimshukuru aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kushirikiana naye kubuni serikali jumuishi.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na waziri wa Nishati Opiyo Wandayi, Seneta wa Siaya Oburu Oginga, wabunge, wawakilishi wadi, viongozi wa dini na viongozi wengine.