Droo ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 17 yabainika

Itakuwa mara ya kwanza kwa fainali hizo kushirikisha mataifa 24 kutoka 16, yaliyoshiriki makala ya mwaka jana katika Jamhuri ya Dominica.

Dismas Otuke
1 Min Read

Waakilishi wa Afrika watakuwa na kibarua kigumu kufuzu kwa hatua ya mwondoano, kufuatia kuandaliwa kwa droo ya makundi ya makala ya tisa ya Kipute cha Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17 nchini Morocco, baadaye mwaka huu.

Wenyeji Morocco wamo kundi A pamoja na miamba Brazil, Costa Rica na Italia, kulingana na droo iliyoandaliwa jana usiku jijini Rabat.

Itakuwa mara ya kwanza kwa fainali hizo kushirikisha mataifa 24 kutoka 16, yaliyoshiriki makala ya mwaka jana katika Jamhuri ya Dominica.

Kulingana na droo hiyo, kundi B linasheheni mabingwa watetezi Korea Kaskazini, Cameroon, Mexico na Uholanzi.

China, Ecuador, Marekani na Norway zimejumuishwa kundi C, nalo kundi D lina Canada, Ufaransa, Nigeria na Samoa.

Uhispania wamerushwa kundi E pamoja na Colombia, Côte d’Ivoire na Korea Kusini, huku kundi F likiwa na Japan, New Zealand, Paraguay, na Zambia.

Timu mbili bora kutoka kila kundi na nne bora zitakazomaliza katika nafasi ya tatu kutoka makundi yote, zitafuzu kwa robo fainali.

Kipute hicho kitaandaliwa katika viwanja vinne jijini Rabat, kati ya Oktoba 17 na Novemba 8 mwaka huu.

Share This Article