Derby ya Mashemeji baina ya Gor Mahia na AFC Leopards, iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu, ghamu na hamamu uwanjani Raila Odinga, iliishia sare ya bao moja Jumatatu jioni .
Wenyeji Gor walichukua uongozi dakika ya 31 kupitia kwa Austin Oduor, kabla ya Bernard Wanyama, kusawazishia wageni Ingwe dakika ya 50.
Ilikuwa sare ya pili mtawalia kwa timu hizo mbili baada ya kuambulia sare kappa, katika duru ya kwanza uwanjani Nyayo mwezi Machi mwaka huu.
Matokeo hayo yamedidimiza matumaini ya Gor kuhifadhi taji ya Ligi Kuu nchini msimu huu, wakilazimika kushinda mechi mbili zilizosalia dhidi ya Ulinzi Stars na Police FC,na kutarajia kuwa Police watapoteza mechi zote mbili, ili kuvishwa ubingwa kwa mara ya 22.

Gor almaarufu K’ogalo, wameratibiwa kuwatembelea Ulinzi tarehe 11 mwezi huu, kabla ya kufunga msimu dhidi ya Police tarehe 15 mwezi huu.
Police, kwa upande wao, wanahitaji tu pointi moja kutokana na mechi mbili dhidi ya Shabana na Gor, kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.
Police wangali wanashikilia kukutu uongozi wa Ligi Kuu ya FKF kwa pointi 61, kutokana na mechi 32, wakifuatwa na Gor Mahia kwa alama 55 sawia na Tusker FC walio katika nafasi ya tatu.