Gavana wa Kwale Fatuma Achani amesema kuwa sekta ya uvuvi na uchumi wa samawati katika kaunti hiyo imeimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine ya Pwani.
Akiwahutubia wakazi wa eneo la Nzovuni, Kinango, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Madaraka, Gavana Achani alieleza kuwa mafanikio haya yamechangiwa na ushirikiano mzuri kati ya serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti, na wafadhili hususan Benki ya Dunia, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta ya uvuvi.
“Hadi kufikia sasa, serikali ya kaunti imetoa boti 50 za kisasa za uvuvi na kufanikisha ujenzi wa bandari ndogo tisa za kisasa za samaki,” alisema Gavana Achani.
Aliongeza kuwa bandari hizo ndogo — zilizoko katika maeneo ya Tsunza, Mwaepe, Waa, Tiwi, na Vanga — zimeboreshwa kwa kuwekewa majokofu ya kisasa na vifaa vingine vya kuhifadhia samaki pamoja na bidhaa nyingine za baharini.
Aidha, takriban kina mama 1,200 wamepatiwa mafunzo ya uvuvi kama sehemu ya juhudi za kuwawezesha kiuchumi na kuhamasisha ushiriki wao katika sekta ya uchumi wa buluu.