Mwanamuziki wa Marekani Cardi B amefichua gharama kubwa ya kulea wanawe watatu huku akilalamikia hatua ya aliyekuwa mume wake Offset ya kuwasilisha ombi mahakamani la kupatiwa usaidizi wa kifedha na Cardi.
Cardi B wa umri wa miaka 32 na Offset wa miaka 33 wana watoto watatu ambao ni Kulture wa umri wa miaka 6, Wave wa miaka mitatu na Blossom wa miezi minane tu.
Mwanadada huyo ambaye alikuwa analalamika mitandaoni alielezea pesa nyingi ambazo anatumia kulipa karo ya shule, yaya wa watoto wake, dereva wao na mpishi wao akisema Offset huwa hachangii lolote.
Mshindi huyo wa tuzo za Grammy alielezea kwamba karo ya Kulture pekee ni dola elfu 45, kwa mwaka huku ile ya Wave ikiwa dola elfu 35 kwa mwaka. Watoto hao hupatiwa masomo ya ziada nyumbani ambapo mwalimu wao hulipwa dola 250 kwa saa.
Dereva wa watoto hao kulingana na Cardi analipwa dola elfu 10 kila mwezi.
“Wanangu wana mpishi wa kibinafsi ambaye huingia saa moja asubuhi na kutoka saa kumi na moja jioni ambaye ninalipa kwa sababu walioko nyumbani hawana muda wa kupika,” alisema Cardi B.
Aliendelea kusema kwamba yeye ndiye alinunua nyumba anayoishi pamoja na watoto wake na analipia ulinzi wa saa 24 kila siku kwani awali walipokea vitisho vya kiusalama.
Cardi aliwasilisha ombi la talaka Agosti 2024, Februari Offset akawasilisha ombi la kibali cha utunzaji wa pamoja wa wanao watatu akielezea kwamba anakokaa Cardi kunafaa kuwa makazi yao ya msingi.
Alhamisi ripoti ziliibuka kwamba Offset aliwasilisha mabadiliko kwa maombi yake kuhusiana na talaka yao ambapo aliongeza ombi la kupatiwa usaidizi wa kifedha na Cardi B.