Maafisa wa usalama katika kaunti ya Busia, wamewaokoa vijana 30 kutoka kwa walanguzi wa binadamu katika kipindi cha mieizi miwili iliyopita.
Kamanda wa polisi eneo la Magharibi Issa Mahmud alisema wahasiriwa hao walio na umri wa kati ya miaka 14 na 25 walikuwa wameahidiwa kazi katika mataifa ya Ulaya na Amerika.
“Katika muda wa miezi miwili iliyopita, tumewaokoa vijana 30 kutoka kwa walanguzi wa binadamu, walio na umri wa kati ya miaka 14-25. Kutokana na uchunguzi wetu, wengi wao walihadaiwa kwamba watapata kazi nzuri Bara Ulaya na Amerika kupitia barabara,” alisema Mahmud.
Uchunguzi ulibaini kuwa vijana hao walisafirishwa kupitia mataifa ya Uganda, Sudan kusini , Sudan na Libya,ambapo walanguzi hao huitisha pesa kutoka kwa familia zao kabla ya kuwavukisha bahari ya Mediterranean.
Mahmud alisema baadhi ya vijana hao waliondolewa shuleni na maeneo ya umma bila idhini ya wazazi wao.Alionya kuwa yoyote anayejihusisha na ulanguzi wa binadamu atakabiliwa vikali kisheria.