Afisa mmoja mkuu wa Hamas amesema kundi hilo la wanamgambo wa kipalestina halitakubali pendekezo la hivi punde la Amerika la kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel.
Ikulu ya White House ilisema siku ya alhamisi kwamba Israel imekubali pendekezo hilo lililowasilishwa na mjumbe wa Amerika Steve Witkof na kwamba inasubiri tuu uamuzi wa kundi hilo la Hamas.
Vyombo vya habari nchini Israel viliwanuku maafisa nchini humo wakisema mpango huo utatoa fursa ya kuachiliwa huru kwa mateka kumi wanaozuiliwa na Hamas pamoja na miili ya wateka wengine 18 waliofariki katika muda wa siku 60 ambapo mapigano hayo yanatarajiwa kusitishwa, huku wafungwa kadha wa kipalestina pia wakiachiliwa huru na Israel.
Afisa huyo wa Hamas alisema mpango huo haukuzingatia baadhi ya matakwa yake muhimu ikiwemo kusitishwa kabisa kwa mapigano hayo.
Serikali ya Israeli haijasema lolote lakini waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu ameripotiwa kuambia familia za mateka wa nchi hiyo kuwa amekubali mpango huo wa Witkoff. Israel imeweka vizuizi kote huko Gaza na kurejelea mashambulizi dhidi ya Hamas.