Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB sasa linataka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu mauaji ya kutisha ya mapadri wawili wa kanisa hilo.
Maaskofu hao wanataka kubaini kilichochochea mauaji ya Padri James Maina na Padri Alois Bett, wakiomba serikali ichukue hatua za haraka.
Walisema katika taarifa ya Mei 28, 2025 kwamba wamesikitishwa pakubwa na vifo vya ghafla vya wawili hao katika muda wa siku chache.
KCCB ilituma salamu za pole kwa Askofu na waumini wa Dayosisi ya Nyahururu kufuatia kifo cha Padri James Maina na kwa mwenzao wa jimbo la Eldoret kwa kifo cha Padri Alois Bett.
Viongozi hao wa kidini wametaja mauaji ya wawili hao kuwa yaliyoghubikwa na nia mbaya na siri kubwa huku wakilalamikia hali ya ukosefu wa usalama na kukosa usaidizi inayojitokeza kutokana na vitendo vibaya dhidi ya watumishi wa Mungu.
James Maina alifariki akipokea matibabu katika kile kinachoaminika kuwa kisa cha utekaji nyara huku Alois Bett akiuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akirejea kutoka huduma.
Huku wakitetea kazi inayofanywa na mapadri wa kanisa Katoliki, Maaskofu hao wamelalamika pia kuhusu hali ya kudunishwa kwa maisha ya binadamu ambapo visa vya mauaji vinachukuliwa kwa wepesi.