Rais Ruto aomboleza kifo cha Gwiji wa fasihi Ngugi wa Thiong’o

Katika ujumbe wake Rais alisema kwamba Ngugi ameweka kalamu yake chini kwa mara ya mwisho.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameongoza taifa katika kuomboleza kifo cha mwandishi maarufu na msomi mashuhuri Profesa Ngugi wa Thiong’o, akimtaja kuwa “jitu la fasihi ya Kenya” ambaye urithi wake utaishi kwa vizazi vijavyo.

Katika rambirambi zake alizotoa kupitia mtandao wa X, Rais Ruto alieleza huzuni kuu kutokana na kuondokewa na mwandishi huyo mashuhuri, akisema kuwa “ameweka kalamu yake chini kwa mara ya mwisho.”

Akikiri ujasiri wake wa kiakili na uzalendo wake, Rais alitambua kuwa Profesa Ngugi aliendeleza maono ya ukweli, haki na mwamko wa kitaifa kupitia maandishi yake.

“Akiwa jasiri, alileta athari kubwa isiyofutika katika namna tunavyofikiri kuhusu uhuru wetu, haki ya kijamii na matumizi au dhuluma za madaraka ya kisiasa na kiuchumi,” alisema Rais Ruto.

Ngugi wa Thiong’o, anayejulikana kwa kazi zake bunifu kama ‘A Grain of Wheat’ na ‘Decolonising the Mind’, aliheshimiwa sana kwa kuandika kwa lugha yake ya mama kikuyu na kwa ukosoaji wake makini wa uongozi barani Afrika baada ya ukoloni.

Alitajwa mara nyingi kama mshindani stahiki wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi — tuzo ambayo Wakenya wengi waliamini kwa dhati kwamba aliistahili kupatiwa.

Ingawa Tuzo hiyo ya Nobel haikumfikia, Rais Ruto alisisitiza kwamba Ngugi atabaki kuwa “bingwa wa ukombozi na ubunifu wa kifasihi katika mioyo na akili zetu.”

Alikamilisha kwa kutuma salamu za rambirambi kwa familia na kuwaombea faraja na amani katika kipindi hiki cha maombolezo.

Familia ya Thiong’o ilitangaza kifo chake jana Jumatano Mei 28, 2025 jioni ikielezea kwamba aliugua kwa muda mfupi.

Share This Article