Mwigizaji wa Nigeria Sarah Martins alilazimika kuomba msanii tajika wa muziki wa taifa hilo Davido msamaha baada yake kuonekana kutangaza kwamba Davido amefungua hoteli.
Martins alitoa ushauri kwa Davido kupitia akaunti yake ya Instagram akisema anahisi Davido angemfungulia mke wake Chioma hoteli hiyo na labda aipe jina lake kutokana na ujuzi alio nao katika mapishi.
“Haya yanatokana na upendo kwa sababu mimi ni shabiki mkubwa wa Davido. Kiukweli ninahisi kwamba hoteli ya Davido ingefunguliwa kwa ajili ya Chioma na laba hata kuitwa jina lake.” aliandika Martins.
Sarah aliendelea kudhihirisha imani kwamba Davido angeridhia ushauri wake na kutangaza hoteli hiyo ya hadhi ya nyota tano itakayokuwa na jina na mke wake Chioma.
Baadaye alichapisha picha ya mawasiliano kati yake na Davido ambapo kwa ghadhabu Davido alishangaa alichokuwa akizungumzia kwenye chapisho lake.
“Ni nini mbaya na wewe? Hebu futa ujinga huo. Ni hoteli gani nilifungua? Tafadhali futa sasa hivi.” Davido alimwambia Martins katika mawasiliano hayo.
Martins naye alijibu akiomba msamaha huku akijiondolea lawama akisema alipata taarifa zisizo sahihi kutoka kwa mtu aliyemrejelea kama Opeyemi. Aliahidi kuomba msamaha hadharani na alifanya hivyo kwa kurekodi video na kuichapisha kwenye Instagram.
Kwenye video hiyo Sarah Martins alimmiminia Davido sifa kede kede na kuomba msamaha mara kadhaa.