Mwanamuziki wa muda mrefu wa Uganda Bebe Cool ametetea kiasi cha pesa alizolipwa msanii wa Tanzania Diamond Platnumz ambaye alikuwa mtumbuizaji mkuu katika tamasha la Kahawa.
Inaarifiwa kwamba Diamond alilipwa shilingi milioni 750 pesa za Uganda sawa na milioni 26.6 za Kenya, hatua ambayo ilimsababisha Rais wa chama cha kitaifa cha wanamuziki nchini Uganda Eddy Kenzo alalamike.
Kenzo alisema hakufurahishwa na jinsi waandalizi wa tamasha hilo walichukulia wasanii wa Uganda yeye akiwemo. Kulingana naye, Diamond alipatiwa mapokezi ya hadhi ya juu ambapo alitumiwa ndege ya kibinafsi na magari ya kifahari.
Aligusia pia malipo ambayo Diamond alipokea ambayo yalikuwa ya kiwango cha juu ikilinganishwa na wasanii wa nyumbani Uganda.
Katika kujibu malalamishi ya Kenzo, Bebe Cool aliamua kutoa ushauri kwa wasanii wa umri mdogo kama Kenzo ambapo alisema kwamba uwezo wao wa kujitetea katika majadiliano ndio utawasaidia pamoja na thamani ambayo mteja anatarajia kupata kutokana na kazi zao.
Kadhalika Cool, alitetea dhana kwamba wasanii wa ughaibuni huenda wakapatiwa kiwango cha juu cha malipo, akisema sio upendeleo bali ni majadiliano ya kibiashara na thamani ya ushawishi wao.
Msanii huyo alikumbuka jinsi alijitetea wakati chama tawala nchini Uganda NRM kilitaka huduma zake katika mradi wa “Tubonge Nawe” ambapo alielezea bayana pesa ambazo alitaka alipwe.
Kulingana naye, Rais Museveni alikubaliana na pesa nyingi alizoitisha kutokana na nembo yake mradi atekeleze jukumu lake ipasavyo.