Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati, wakiwa na magunia 10 ya bangi, kaunti ya Machakos.
Wawili hao Samuel Baraza Nyongesa mwenye umri wa miaka 38 na Lawrence Onyango, walikamatwa baada ya maafisa hao kupashwa habari na kuwavizia katika kijiji cha Kitanga, kaunti ya Machakos.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI, wawili hao walikwepa mtego wa maafisa hao katika eneo la Lari Flyover kaunti ya Kiambu.
Baada ya gari lao aina ya Toyota Noah lenye nambari za usajili KDN 218A kufanyiwa uchunguzi, bangi hiyo ya thamani ya shilingi Milioni 7.5 ilipatikana.
Kwa sasa bangi na gari hilo zinazuiliwa katika Makao Makuu ya DCI Jijini Nairobi, huku washukiwa hao wakisubiri kufikishwa mahakamani.