Kiongozi wa chama cha National Unity Platform – NUP cha Uganda, Robert Kyagulanyi anayefahamika sana kama Bobi Wine amesema kwamba chama chake kiko tayari kwa uchaguzi mwingine katika eneo bunge la Kawempe Kaskazini.
Haya yanafuatia hatua ya mahakama kuu ya Kampala ya kufutilia mbali ushindi wa Elias Nalukoola katika uchaguzi mdogo uliofanyika Machi 13, 2025.
Katika uamuzi wake, Jaji Bernard Namanya alisema kwamba alipata kwamba uchaguzi mdogo uliofanyika mapema mwaka huu ulikiuka sheria ya uchaguzi wa wabunge na makosa yaliyoshuhudiwa huenda yaliathiri matokeo.
Akizungumza jana Jumatatu katika eneo la Kaskazini mwa Uganda, Bobi Wine alisema kwamba hata ingawa wamepata changamoto hiyo, wamejitolea kurejea kwa wapiga kura na kushinda kwa mara nyingine.
“Alichokifanya Jaji Namaya hakituzuii. Tutakata rufaa lakini mahakama ya rufaa inaweza pia ikakosa haki, lakini tunafurahia kurejea kwa watu wa Kawempe kwa mara nyingine,” alisema Wine.
Kulingana na kiongozi huyo wa NUP uamuzi huo wa mahakama kuu ni dhihirisho la ufisadi uliokita mizizi katika mifumo ya kisheria na ya kisiasa nchini Uganda.
Kyagulanyi analaumu chama tawala National Resistance Movement – NRM kwa kutumia vurugu na pesa nyingi kujaribu kushinda kiti hicho cha ubunge cha Kawempe Kaskazini.
Wadhifa wa ubunge katika eneo hilo la Kawempe Kaskazini ulisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge Muhammad Ssegirinya ambaye aliugua kwa muda.
Ssegirinya alikuwa mwanachama wa National Unity Platform, chama kinachoongozwa na Bobi Wine.